News
MWAUWASA IMEFANYA KAZI NZURI NANSIO
MWAUWASA IMEFANYA KAZI NZURI NANSIO
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amepongeza jitihada za MWAUWASA za kuwafikishia huduma ya majisafi na salama wananchi wa Nansio Wilayani Ukerewe.
Waziri Aweso ametoa pongezi hizo Agosti 12, 2021 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa Maji Muriti -Ihebo unaotekelezwa na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani Ukerewe.
Mradi huo wa Muriti -Ihebo unagharimu Milioni 903.7 na unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 15,000
"Nimeridhishwa na hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama katika Mji wa Nansio," alisema Waziri Aweso.
Mji wa Nansio Wilayani Ukerewe ni miongoni mwa miji inayohudumiwa na MWAUWASA na miji mingine ikiwa ni Magu, Misungwi na Ngudu kufuatia hatua yenye maelekezo ya Serikali kupitia Wizara ya Maji kuiongezea wigo wa eneo la usimamizi katika utoaji wa huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira kama ilivyotangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali GN Na. 670 la Septemba 6, 2019 na GN Na. 70 la Januari 31, 2020.
Aidha, katika hafla hiyo Waziri Aweso alisisitiza kuwa hatokuwa kikwazo katika kuwafikishia huduma ya majisafi na salama wananchi waishio maeneo ya vijijini.
"Niwahakikishie kwamba sintokuwa kikwazo kwa wananchi wa Ukerewe kupata huduma ya majisafi na salama," alisisitiza Waziri Aweso.
Waziri Aweso ameelekeza watendaji Sekta ya Maji kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa kwa ubora na kasi zaidi ili kuwaondolea adha ya ukosefu wa huduma ya maji wananchi.