News

Posted On: Jul, 13 2022

SERIKALI INATAMBUA JITIHADA ZA MWAUWASA

News Images

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amesema Serikali inatambua jitihada za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA) katika kuhakikisha huduma inafika kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza.

Mhandisi Gabriel amesema hayo hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau kilicholenga kujadili mradi wa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania kupitia MWAUWASA na Serikali ya Uholanzi, kupitia Mamlaka za Maji za Uholanzi chini ya mpango mahsusi wa WaterWorX.

Mhandisi Gabriel alipongeza jitihada za MWAUWASA na kubainisha kuwa zinakwenda sambamba na azma ya Serikali katika kuwaletea wananchi wake maendeleo endelevu.

“Kama mnavyofahamu Rais wetu, Mama yetu mpendwa Mhe. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza ushirikiano na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi. Mhe. Rais mara zote amekuwa akisisitiza umuhimu wa kushirikisha na kushirikiana na wadau mbalimbali kwenye miradi ya kijamii na ya maendeleo kwa dhamira ya kuleta tija kwa wanufaika ama walengwa na hapa tutakuwa na miradi endelevu,” alisema.

Hata hivyo alisema licha ya jitihada hizo za MWAUWASA bado kuna changamoto ya upotevu wa maji maeneo yote yanayohudumiwa na MWAUWASA na hivyo kuwasihi wadau kujadili pia namna bora ya kukabiliana na changamoto hiyo.

“Wadau wote mliohudhuria hapa ninawasihi kuupa mkutano huu umuhimu wa kipekee kwa mustakabali wa maendeleo ya wana Mwanza kwenye Sekta ya Maji hasa ikizingatiwa kwamba maji ni uhai, hivyo basi mkutano huu ni muhimu sana kwetu,” alisisitiza.