News
DAWASA YAIMARISHA UHUSIANO NA MWAUWASA

Baadhi ya watumishi kutoka Idara ya Uzalishaji na Usambazaji Maji ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wametembelea MWAUWASA kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika sekta ya uzalishaji na usambazaji wa maji.
Watumishi hao kutoka DAWASA walipata fursa ya kutembelea vyanzo vya maji na mitambo ya kuchuja na kutibu maji ya MWAUWASA katika maeneo ya Capri Point na Butimba.
Ziara hiyo ya mafunzo imelenga kuangazia mifumo ya uzalishaji maji, usimamizi wa vyanzo vya maji, teknolojia za kisasa za kutibu maji, pamoja na mbinu bora za usambazaji maji kwa wateja ili kuhakikisha huduma bora na endelevu kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kiongozi wa timu ambaye ni Mkurugenzi wa Usambazaji Maji DAWASA, Mhandisi Leonard Msenyele amesema kuwa ziara hiyo imewapa fursa ya kujifunza mbinu mpya na suluhisho za kiufundi zitakazosaidia kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa MWAUWASA, Mhandisi Salim Losindilo ameipongeza DAWASA kwa jitihada zake za kutafuta maarifa zaidi kupitia ushirikiano wa kitaalamu, akisisitiza kuwa uhusiano kama huu unaleta maendeleo chanya katika sekta ya maji kitaifa.