News

Posted On: Jan, 17 2024

DC ILEMELA AONYA WANAOELEKEZA MAJI YA MVUA KWENYE MFUMO WA MAJITAKA

News Images

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hassan Masala ametoa wito kwa wananchi kuacha kuunganisha mfumo wa maji ya mvua katika mabomba (mifumo) ya majitaka.

Ametoa rai hiyo hivi leo Januari 14, 2024 alipofanya ziara maalum Kata ya Kirumba ili kuhamasisha wananchi suala la usafi ikiwa ni nyenzo muhimu ya kujilinda na kutokomeza maradhi ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

"Zipo baadhi ya nyumba ambazo wameunganisha mifumo ya maji ya mvua na mifumo ya majitaka na hivyo kusababisha ongezeko kubwa la maji kwenye mifumo ya majitaka na imepelekea mfumo wa majitaka kuelemewa," amebainisha.

Ameielekeza MWAUWASA kubaini nyumba ambazo zimeunganisha maji ya mvua na mfumo ili kutoa elimu na kuchukua hatua stahiki sambamba na kukagua miundombinu yake ya majitaka.

"MWAUWASA natambua kuna jitihada mnaendelea nazo ninawaelekeza kufuatilia mfumo wenu kuanzia kwa wananchi hadi hapa mnapokusanyia majitaka ili kuepuka uvujaji wa chemba za majitaka, jitihada za kuimarisha kituo hiki cha kupokelea majitaka hapa eneo la Mwaloni ziende sambamba na ukaguzi wa mfumo mzima na tupate taarifa," ameelekeza.

Mhe. Masala vilevile ametoa wito kwa wananchi kuacha mara moja tabia ya kutiririsha ovyo majitaka kipindi hiki cha mvua suala ambalo amesema ni kichocheo cha maradhi ya mlipuko.

Ametoa wito kwa wananchi wote kuhakikisha wanazingatia suala zima la usafi binafsi wa mtu mmoja mmoja na mazingira kwa ujumla na kuzingatia maelekezo ya wataalam wa afya ili kupambana na maradhi ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.