News
JAMII YASHIRIKISHWA USULUHISI WA MIGOGORO KWENYE MIRADI YA MAJI

Wataalam wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) wamekutana na viongozi wa mitaa 30 pamoja na wajumbe wao katika kikao kazi kilichofanyika leo tarehe 23 Agosti 2025.
Lengo kuu la kikao hicho ni kuwawezesha viongozi hao wa mitaa kuelewa na kushiriki kikamilifu katika utatuzi wa migogoro ya maji inayojitokeza katika jamii, hasa migogoro ya ngazi ya chini inayoweza kutatuliwa kabla ya kufikishwa ngazi ya juu.
Kikao hicho kilifunguliwa na Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Salim Lossindilo ambaye aliwataka viongozi hao kuwa kiungo muhimu kati ya wananchi na MWAUWASA.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano, Bi. Vivien Temu aliwahimiza viongozi hao kujitoa zaidi katika kutatua changamoto zinazohusu huduma ya maji, hasa kwenye maeneo yanayohusiana na utekelezaji wa miradi ya maji.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyamazobe, Ndugu Mohamed Kalimanzira, ameipongeza MWAUWASA kwa jitihada hizo na kusema kuwa elimu hiyo imesaidia sana kuwajengea uwezo wa kutatua migogoro ndani ya jamii kwa ustawi wa huduma ya maji.