News

Posted On: Dec, 30 2021

​​Maafisa Ununuzi na Ugavi watakiwa kutokuwa kikwazo katika utekelezaji wa miradi ya maji

News Images

Maafisa Ununuzi na Ugavi watakiwa kutokuwa kikwazo katika utekelezaji wa miradi ya maji.

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka Maafisa Ununuzi na Ugavi kutokwamisha Miradi ya maji kwa kuwa na mlolongo mrefu na Michakato isiyo ya lazima wakati wa utekelezaji wake.

Waziri Aweso ametoa maelekezo hayo Mkoani Mwanza Desemba 12, 2021 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Wakuu wa Vitengo vya Ununuzi na Ugavi wa Wizara ya Maji na na Taasisi zake .

“Michakato isiyo ya lazima achaneni nayo, tushirikiane kuhakikisha hatui kikwazo kwenye utekelezaji wa miradi ya maji kwenye maeneo yetu, tuhakikishe nidhamu kazini na kutenda haki," alielekeza Waziri Aweso.

Alisema vitengo vya Ununuzi na Ugavi ni muhimu kwenye Wizara ya Maji na kwamba maendeleo ya Sekta ya maji yanaanza na wote hivyo ushirikiano baina ya idara, vitengo na hata taasisi ni jambo la kupewa kipaumbele.

“Tunawajibu wa kutimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani na kuhakikisha asilimia ya upatikanaji maji mijini inafika asilimia 95 na asilimia 85 vijijini ifikapo mwaka 2025 na tukitaka kufika huko lazima tuwe wamoja, tupendane na tusaidiane,” alisema Waziri.

Waziri Aweso aliwataka wakuu hao wa vitengo vya Ununuzi na Ugavi kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa na inapaswa kukamilika kwa wakati.

“Twendeni tukamsaidie Raisi wetu, twendeni tukasaidie Serikali Yetu, twendeni tukasaidie Wizara yetu kutokana na taaluma mlizonazo," alisisitiza Waziri Aweso.

Aidha, alimpongeza Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi wa MWAUWASA, Poas Kilangi ambaye ni Mwenyekiti wa Kikao hicho kwa maandalizi mazuri pamoja na uongozi wake na aliwaasa wajenge utamaduni wa kusaidiana na kushirikiana ili kuleta mafanikio zaidi katika wizara.

Vilevile alizungumzia suala la wakandarasi wa maji na alisisitiza kuwa wakandarasi walioharibu kazi kwenye Wizara ya maji wasipewe kazi nyingine.