News

Posted On: Jan, 28 2025

MBUNGE WA KWIMBA ARIDHISHWA NA KASI YA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI NGUDU

News Images

Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mhe. Shanif Mansoor ametembelea eneo la utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji mtandao wa maji na ufufuaji Visima eneo la Kilyaboya na kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo.

Akiwa eneo la Mradi katika Visima vya Kilyaboya Mhe. Mansoor amesema hatua iliyofikiwa ni nzuri na inaleta matumaini kwa wakazi wa Mji wa Ngudu.

"Nashukuru Mradi unakwenda vizuri, niliongea na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso na akatuahidi kutusaidia kupata mradi huu, tulisema tuanze na ufufuaji wa Visima hivi na sasa naona tupo katika hatua nzuri, niwaombe MWAUWASA baada ya Mradi kukamilika ongezeni kasi ya kuwaunganishia huduma Wananchi wengi zaidi ili wanufaike na Mradi huu" ameeleza

Kwa upande wake Meneja wa Miundombinu MWAUWASA Mha. Stanley Mwasawala amesema Mradi huo sasa umefikia asilimia 56% za utekelezaji na ukikamilika utaimarisha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Mji wa Ngudu na hivyo Wananchi wengi zaidi watanufaika.

"Tunaenda kuwafikia wananchi wengi zaidi baada ya kumaliza utekelezaji wa mradi huu, kwa sasa tunapata maji nusu ya mahitaji Lita laki 6 kwa siku na mradi huu utaongeza uzalishaji kwa Lita laki 6 na hivyo tutafikia mahitaji ya Lita Milioni 1.2 ya maji kwa siku"

Katika hatua nyingine Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano MWAUWASA Vivien Temu ameeleza kuhusu ushirikishwaji wa Jamii kuhusu huduma ya maji kwa ujumla katika Mji wa Ngudu.

"Tunaendelea kuhakikisha wananchi wanapata taarifa zote muhimu kuhusu utekelezwaji wa mradi huu na huduma zinazotolewa, tutaendelea kufanya vikao na kuwafikia zaidi Wananchi na Wadau wetu ili sote twende pamoja kila hatua" amefafanua.

Mradi wa ufufuaji Visima na uboreshaji wa Mtandao wa Maji Ngudu utazalisha maji Lita laki 6 (600,000Ltrs) na unahusisha ufufuaji wa Visima viwili eneo la Kilyaboya na uboreshaji wa mtandao wa maji kwa urefu wa KM 4.5 kwa gharama ya TZS 300,000,000.00