News

Posted On: Dec, 30 2021

MENEJIMENTI YA MWAUWASA YATEMBELEA MRADI WA MAJI KYAKA/BUNAZI WILAYANI MISSENYI MKOA WA KAGERA.

News Images

MENEJIMENTI YA MWAUWASA YATEMBELEA MRADI WA MAJI KYAKA/BUNAZI WILAYANI MISSENYI MKOA WA KAGERA.

Menejimenti ya MWAUWASA chini ya Mkurugenzi wake, Mhandisi Leonard Msenyele ilifanya ziara ya siku moja Desemba 12, 2021 ya kutembelea mradi wa Kyaka Bunazi unaosimamiwa na MWAUWASA kwa niaba ya Wizara ya Maji ili kujionea hatua iliyofikiwa.

Mradi huu ulianza kutekelezwa Tarehe 8 Juni, 2020 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Desemba, 2021.

Mradi wa Kyaka/Bunazi unatarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya Efu Sabini na Tano kutoka maeneo ya Kyaka, Bunazi na maeneo mengine ya jirani.

Mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa gharama ya Shilingi Bilioni 15.7 na unatekelezwa katika sehemu mbili ambapo sehemu moja inatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya China Civil Engineering Construction Company (CCECC) na nyingine inatekelezwa na Wataalam wa Ndani yaani Force Account.

Utekelezwaji wake unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji chenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 7 kwa siku, ujenzi wa chujio/mtambo wa kutibu maji, ujenzi wa ofisi, maabara na nyumba za watumishi, ujenzi wa bomba kuu la kusafirisha maji kutoka kwenye chanzo hadi kwenye mtambo wa kutibu maji lenye urefu wa kilomita 1.7km, ujenzi wa mabomba ya usambazaji maji yenye urefu wa kilomita 74.5, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji (viosk) 10 na ujenzi wa maeneo kwa ajili ya zimamoto vituo 10.