News

Posted On: Sep, 07 2021

MWENGE WA UHURU 2021 WARIDHISHWA NA MATUMIZI YA FEDHA MRADI WA MAJI NYEGEZI

News Images

MWENGE WA UHURU 2021 WARIDHISHWA NA MATUMIZI YA FEDHA MRADI WA MAJI NYEGEZI

Kiongozi wa mbio maalumu za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2021 Luteni Josephine Mwambashi ameridhishwa na matumizi ya fedha katika mradi wa maji wa Majengo Mapya Nyegezi Wilayani Nyamagana.

Luteni Mwambashi alibainisha hayo Julai 6, 2021 alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika mradi huo na aliweka bayana kwamba nyaraka za mradi zinaakisi gharama halisi iliyotumika na aliipongeza MWAUWASA kwa usimamizi mzuri wa mradi.

Akizungumzia hali ya huduma kwa ujumla kwa wanufaika wa mradi, Luteni Mwambashi aliwasihi kuwa na subira wakati wataalam wanaendelea na zoezi la kuwaunganishia huduma kutoka kwenye mradi huo.

"Ndugu zangu tupo hapa kwenye mradi wa maji, ninafahamu umekwishaanza kutoa huduma ya maji kwa baadhi ya wananchi kwa sababu mradi huu unahusisha sana kuwaunganisha maji wananchi moja kwa moja katika makazi yao kwahiyo ambao bado hamjafikiwa endeleeni kuvuta subira mtafikiwa," alisema Luteni Mwambashi.

Pia alisema changamoto iliyojitokeza ya baadhi ya wananchi kutounganishwa kwa wakati ilisababishwa kukosekana kwa dira (mita) za maji kutokana na mlipuko wa COVID-19 hasa ikizingatiwa kwamba mita hizo hutengenezwa nje ya Tanzania.

"Wananchi wakiona tenki kubwa namna hii na lipo karibu halafu hawapati maji inakuwa ni changamoto lakini ndugu zangu tunafahamu wakazi wa Mwanza kuwa tupo wengi na tenki hili lina hudumia watu wengi kwahiyo maji haya yanakuwa ya mgao kutokana na mahitaji mengi ya wananchi nisisitize kwamba zoezi lianze kwa kuwahudumia wale ambao fomu zao zimekamilika," alielekeza.

Akisoma taarifa ya mradi huo kwa Luteni Mwambashi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Mhandisi Leonard Msenyele, Meneja Miradi wa MWAUWASA, Mhandisi Gogadi Mgwatu alisema utekelezaji wa mradi umekamilika kwa asilimia 100 na utawanufaisha wananchi 10,500 kutoka Kata za Nyegezi, Mkolani na Buhongwa wilayani Nyamagana.

Mhandisi Mgwatu alisema mradi unathamani ya shilingi bilioni 3.7 ambayo ni fedha kutoka Serikali Kuu na wahisani wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Taasisi ya watu wa Ufaransa (AFD).

Mradi huu wa tenki la Majengo mapya ni sehemu ya mradi mkubwa uliotekelezwa na mkandarasi JR International wenye lengo la kuboresha huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza.