News

Posted On: Oct, 10 2022

OPARESHENI MAALUM

News Images

Oktoba 7, 2022

Mmliki wa Tema Hoteli iliyoko Mtaa wa Nyabulogoya Kata ya Nyegezi Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza Ebeneza Foya, anatuhumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuiba maji kwa kujiunganishia kinyume na utaratibu baada ya kuwa amesitishiwa huduma ya maji Januari 2021.

Suala hili lilidhihirika baada ya wananchi wa Mtaa wa Nyabulogoya kutoa malalamiko ya kukosa huduma ya maji kutokana na mmiliki wa hoteli hiyo kukata mabomba yao na kujiunganishia maji.

Mwanasheria wa MWAUWASA Oscar Twakazi anafafanua hali halisi ya tukio hilo na anasema mteja huyo alisitishiwa huduma ya maji kutokana na kuwa na malimbikizo ya madeni ya maji.

"Kipindi cha nyuma tuliwahi kumkamata lakini tulitumia Sheria ya Maji kumuadhibu na alitozwa penati ya shilingi Milioni moja na nusu ambayo aliilipa, tukafanya makisio ya matumizi ya maji ambayo yalifikia zaidi ya milioni mbili ambazo ziliingizwa kwenye akaunti yake kama deni la maji na hadi sasa fedha hizo hajazilipa," anafafanua Twakazi

Anasema kutokana na Sheria namba 5 ya Mwaka 2019 ya Maji na Usafi wa Mazingira adhabu ya chini ya mtu aliejiunganishia maji ni milioni 2 na ya juu ni milioni 50.

Twakazi amesema tayari taarifa hizi zimefika Polisi katika kituo cha Polisi Igogo na taratibu za kufungua kesi zimefanyika.

Mkuu Msaidizi wa Kanda ya Nyegezi upande wa Mauzo na Makusanyo, Stephen Otonde amesema Akaunti ya Ebeneza Foya wakati inasitishiwa huduma ilikuwa inadaiwa 907,467 ambapo wastani wa matumizi ilikuwa kati ya 190,000 hadi 200,000 kwa mwezi

Akizungumza kwa niaba ya wananchi Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyabulogoya Renatusi Manyanga, amesema amekuwa akipata malalamiko ya kukosa maji kutoka kwa baadhi ya wakazi hatua iliyopelekea kukaa kikao na baraza la Wazee kwaajili ya kufuatilia jambo hilo na walimwagiza kwenda kwa Mkurugenzi wa MWAUWASA kutoa taarifa ya ukosefu wa maji.

"Nilipeleka taarifa kwa Mkurugenzi akaniahidi kuwa atatuma timu yake ili ije ifanye uchunguzi na leo nashukuru sana wamefika na wamejionea wizi wa maji unaofanywa na Mmliki wa Tema Hoteli unaosababisha Wananchi kushindwa kupata maji," alisema Manyanga

Jitihada za kumpata Mmliki wa Tema Hoteli Ebeneza Foya, ziligonga mwamba baada ya kupigiwa simu iliita na hakupokea.