News

Posted On: Aug, 12 2025

RAIS SAMIA AZINDUA MRADI WA MAJI BUTIMBA

News Images

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa chanzo cha maji Butimba wenye thamani ya TZS Bilioni 71.7 uliopo eneo la Butimba Jijini Mwanza .

Mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha Maji Lita Milioni 48 kwa siku utanufaisha wananchi zaidi ya 450,000 wa Wilaya za Nyamagana, Ilemela na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Magu.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi Mhe. Rais Amesema Chanzo hicho kimeanza kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa Jiji la Mwanza na kutoa wito wa kutunza na kulinda vyanzo na miundombinu ya maji ikiwemo Mradi huo uliotumia uwezekezaji mkubwa kwa manufaa ya sasa na baadaye.

"Mara kadhaa nimekua nikipita maeneo jirani na hapa na kupewa taarifa kuwa mradi unatekelezwa na kwa Jiji la Mwanza kilio kimekua ni upungufu wa maji, nafurahi kuona leo hii mradi umekamilika" amesema Mhe. Rais Dkt Samia.

Aidha ameongeza kuwa Serikali imejipanga kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji na kwamba baada ya mradi huo kukamilika serikali inaendelea na ujenzi wa Matenki na miundombinu ya usambazaji maji ili huduma izidi kuimarika.

Kadhalika, mbali na kuipongeza Wizara ya Maji kupitia MWAUWASA kwa usimamizi mzuri wa Mradi ameonya watendaji wa Mamlaka kutobambikia bili Wateja na kuwahimiza wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali kwa kulipia bili za maji kwa wakati.

Kwa upande wake Mhe. Jumaa Hamidu Aweso (Mb) Waziri wa Maji amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi ya Maji na Usafi wa Mazingira na kwamba sasa Wizara ya Maji imekua na ufanisi katika utekelezaji wa miradi kwa kuifanikisha miradi chechefu iliyokwama kwa muda mrefu.

Upatikanaji wa huduma ya maji kwa sasa Jijini Mwanza umefikia asilimia 87 na hivyo kufikia lengo la Serikali la kufikia asilimia 85 za upatikanaji wa huduma ya maji Mijini.