News
SERIKALI IMEJIPANGA KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI MWANZA
SERIKALI IMEJIPANGA KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI MWANZA
Serikali imesema changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Mwanza itamalizika baada ya kukamilika kwa miradi ya kimkakati ya maji inayoendelea kutekelezwa.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Paul Makonda wakati wa ziara alipotembelea eneo la mradi wa ujenzi wa tenki la maji la Fumagila lenye lita milioni 10 ambalo ni sehemu ya mradi mkubwa wa matenki matano, vituo vya kusukuma maji na ulazaji wa mabomba makuu.
Mhe. Makonda amesema itakapokamilika miradi ya upanuzi wa vyanzo vya kuzalisha maji vya Capripoint na Butimba na mradi wa matenki upatikanaji wa maji utaongezeka na huduma itaimarika huku akisisitiza uwajibikaji kwa watendaji ili miradi ikamilike kwa wakati na kunufaisha wananchi.
Awali akiwasilisha taarifa kwa Mhe. Waziri Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Mha. Leonard Msenyele amesema kwa sasa uzalishaji wa maji Mwanza ni Lita milioni 138 huku Mahitaji yakiwa zaidi ya milioni 290 lakini baada ya miradi hiyo kukamilika uwezo wa uzalishaji utafikia kiasi cha lita Milioni 322 na hivyo kukidhi mahitaji ya wakazi wa jiji la Mwanza.
Aidha, akieleza maendeleo ya ujenzi wa tenki la maji Fumagila Meneja wa Miradi MWAUWASA mhandisi Nuhu Said amesema ujenzi wa tenki umefikia asilimia 75 huku ukitarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 80,000 wa maeneo ya kata za Kishiri, Kanenwa, Bukaga, Fumagila na maeneo Jirani.
Kwa ujumla mradi huo wa ujenzi wa matenki matano yenye jumla ya lita Milioni 31, vituo viwili vya kusukuma maji na ulazaji wa mabomba makuu kwa urefu wa Km 40.5 umefikia asilimia 83 uki gharimu TZS Bilion 46 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.