News

Posted On: Sep, 07 2021

TUNAKUSIKILIZA NA KISHA TUNATEKELEZA

News Images

TUNAKUSIKILIZA NA KISHA TUNATEKELEZA

Katika kuhakikisha tunaboresha huduma ya maji kwenye maeneo tunayohudumia, tumedhamiria kukutana na wadau mbalimbali ili kujadili namna bora ya uboreshaji wa huduma.

Hivi leo tarehe 30 Julai, 2021 tumekutana na kufanya mazungumzo na Madiwani wa Halmashauri za Nyamagana na Ilemela na kujadiliana namna bora ya kuboresha huduma ya maji kwenye Kata zao.

Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa MWAUWASA (Maji House) Julai 30, 2021 chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi MWAUWASA, Christopher Gachuma na Wajumbe wa Bodi.

Katika kikao hicho, Menejimenti ya MWAUWASA ilishiriki kikamilifu ili kupata mawazo ya wadau ya namna bora ya kuboresha huduma.

Awali kabla ya kikao, Waheshimiwa Madiwani walipata fursa ya kutembelea Chanzo cha Maji na Kituo cha Tiba ya Maji Capripoint ili kuongeza uelewa wa hatua mbalimbali za usafishaji na utibuji wa maji ghafi kutoka ziwani kabla ya kuwasambazia wananchi (wateja) bombani.

Kwa nyakati tofauti, Madiwani walipongeza jitihada na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na MWAUWASA katika kuhakikisha huduma ya maji inaimarika sambamba na kutoa wito wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ili kuondokana na adha ya maji kwenye maeneo mbalimbali.

Tunashukuru kwa mawazo tuliyopokea kutoka kwa wadau wetu (Waheshimiwa Madiwani) na tunaahidi ufanisi, ubunifu na weledi katika utekelezaji wake.

Tunaendelea kukutana na wadau kwa makundi tofauti na kwa nyakati tofauti ili kujadili changamoto zilizopo sambamba na kupata mawazo ya namna bora ya kuboresha huduma ya maji kwenye maeneo yote tunayohudumia.