News

Posted On: Jan, 28 2025

UKAGUZI WA MIUNDOMBINU YA UZALISHAJI NA HUDUMA KWA JAMII

News Images

Katika jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa Jiji la Mwanza na viunga vyake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Neli Msuya amefanya ziara katika Chanzo cha uzalishaji maji cha Butimba kwa lengo la kukagua shughuli za uzalishaji maji zinazoendelea kutekelezwa katika Chanzo hicho na baadae kutembelea Wateja kujionea hali ya upatikanaji wa huduma katika maeneo yao.

Katika ziara hiyo ya Januari 20 ,2025 ambayo ni muendelezo wa utaratibu wake wa kukagua miundombinu katika eneo la kihuduma la MWAUWASA, Mkurugenzi Neli amekagua Mitambo ya uzalishaji maji pamoja na kupatiwa maelezo kuhusu maendeleo ya shughuli za uzalishaji maji katika Chanzo hicho.

Aidha, akiwa katika Chanzo hicho Mkurugenzi Neli ameisisitiza timu ya uzalishaji iliyoongozwa na Msimamizi wa Chanzo hicho Mhandisi Joseph Malimi kuhakikisha Mitambo inafanya kazi kwa ufanisi wake muda wote ili kiwango cha maji kinachotarajiwa kuzalishwa kwa kila siku kifikiwe na kunufaisha wananchi wanaohudumiwa na Chanzo hicho.

Vilevile, baada ya kukagua kazi za uzalishaji Mkurugenzi Neli alitembelea eneo la Buguku na kukagua hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa maeneo hayo.

Akiwa katika maeneo hayo alipata fursa ya kuzungumza na wateja pamoja na watoa huduma wa MWAUWASA lengo ikiwa ni kusisitiza ulipaji wa ankara, upatikanaji wa maji ya uhakika na uimarishwaji wa huduma bora kwa wananachi.