News

Posted On: Apr, 03 2024

USHIRIKIANO NA WADAU WA MAENDELEO

News Images

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo kutoka Nchini Ujerumani imejipanga kuboresha Miundombinu ya Usafi wa Mazingira kupitia Mradi wa Green and Smart Cities 'SASA' ikiwa ni mpango madhubuti wa kuimarisha usafi na utunzaji wa Ziwa Victoria.

Ujumbe kutoka Ubalozi wa Ujerumani umeambatana na Wadau wanaoshiriki katika utekelezaji wa mradi huo Leo 22.03.2024 kutembelea Mto Mirongo katika Kata ya Mirongo Wilayani Nyamagana ikiwa ni moja ya maeneo yaliyoainishwa kufanyiwa kazi katika utekelezaji wa Mradi.

Wakiwa katika eneo hilo wamejionea namna uchafuzi wa mto huo unavyoweza kuchangia uchafuzi wa Mazingira ikiwemo ziwa Victoria na kusababisha athari mbalimbali hasa katika kipindi cha Mvua.

Wadau hao wamejadili namna wanavyoweza kushirikiana kwa pamoja na Wafadhili ili kuweza kuimarisha Miundombinu katika eneo hilo na kupunguza athari zinazoletwa na uchafuzi wa Mto huo katika mazingira na ziwa Victoria.

Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Ndg. Neli Msuya ameueleza ujumbe huo kuhusu mipango ya Mamlaka katika kuendeleza uboreshaji wa Miundombinu ya Usafi wa Mazingira kupitia utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya Usafi wa Mazingira.

Aidha, Amewaeleza pia kuhusu Mipango ya Mamlaka katika kuhakikisha jamii inashirikishwa vyema katika utekelezaji wa Miradi na Matumizi sahihi ya miundombinu ya utunzaji wa Mazingira.

Ujumbe huo umeahidi kuimarisha ushirikiano na MWAUWASA katika kuhakikisha Uimarishaji wa Usafi wa Mazingira pamoja na utunzaji wa ziwa Victoria.

#Kaziinaendelea 💦