News
USHIRIKIANO WA TANZANIA NA UMOJA WA ULAYA KUENDELEA KUIMARISHA HUDUMA YA MAJI MWANZA
Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) unatarajiwa kuendelea kuimarisha huduma ya maji jijini Mwanza kupitia uwekezaji kwenye miradi ya maji na usafi wa mazingira. Hayo yamebainika Ijumaa, Oktoba 30, 2026, wakati wa ziara ya ujumbe wa Umoja wa Ulaya ulioongozwa na Balozi wa umoja huo nchini Tanzania, Jean-Marc Pisani, akiwa na Balozi wa Ufaransa, Jean Baptiste Jeangène, pamoja na washirika wengine wa timu hiyo, walipotembelea mtambo wa maji wa Butimba.
Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele, amesema mradi wa LVWATSAN, uliozaa mtambo wa Butimba uliozinduliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2025, unaingia Awamu nyingine baada ya mkataba wa ufadhili kusainiwa. Ufadhili huo, wa ruzuku na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa Ulaya, unawezesha upatikanaji wa fedha takriban euro milioni 166 kuongeza uzalishaji wa maji wa chanzo cha Butimba kutoka lita milioni 48 hadi milioni 170 kwa siku, sambamba na uboreshaji wa mifumo ya usambazaji maji, miradi ya majitaka, mafunzo kwa wataalamu kuwajengea uwezo (capacity building) na matumizi ya nishati ya jadidifu ya jua ili kuhakikisha huduma ya uhakika kwa kuwa na mbadala inapotokea changamoto za umeme .
Aidha, akitoa taarifa kwa ujumbe wa EU, Mhandisi Msenyele ameeleza kuwa kutokana na ukuaji wa kasi wa Jiji la Mwanza na kuongezeka kwa wakazi, mahitaji yau maji yameendelea kuongezeka kwa kasi hiyohiyo. Ameeleza kuwa mahitaji ya maji kwa sasa yanafikia takribani lita milioni 293 kwa siku, huku uzalishaji ukiwa chini ya kiwango hicho. Amesema miradi hiyo mikubwa inayokuja itapunguza changamoto ya maji kwa wana-Mwanza kwa kiasi kikubwa akigusia pia mwelekeo wa Serikali wa Dira 2050.
Kwa upande wake, Balozi Pisani amesema kupitia programu ya Global Gateway, EU inaunganisha uwekezaji na utaalamu wa Ulaya na vipaumbele vya Tanzania ili kuleta suluhisho la vitendo kwenye huduma za maji na usafi wa mazingira. Ameeleza kuwa teknolojia kutoka Ulaya na ushirikiano wa nchi wanachama, zikiwemo Ufaransa, Ubelgiji, Ujerumani na Denmark, pamoja na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), ni nguzo ya ushirikiano huo, ambao Dira ya Tanzania 2050 inaupa msingi imara