News

Posted On: Aug, 12 2025

WATUMISHI MWAUWASA WAPEWA NONDO UTOAJI HUDUMA BORA

News Images

Mtaalamu wa masuala ya saikolojia na mahusiano kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, *Dkt. Chris Mauki*, ametoa mafunzo kwa Sehemu ya watumishi wa *MWAUWASA*, ikiwa ni mkakati wa mamlaka kuboresha utoaji huduma kwa wananchi kupitia mpango maalum wa kuwajengea uwezo watumishi.

Awamu hiyo ya kwanza ya mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka yamelenga kuongeza *uwezo wa mawasiliano na wateja, uwajibikaji. Mafunzo pia yalijikita katika umuhimu wa ubunifu katika kazi, kuongeza ufanisi, huduma bora kwa wateja na kukuza mshikamano miongoni mwa watumishi* ili kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, *Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Neli Msuya*, amesisitiza umuhimu wa watumishi kuzingatia yale waliyojifunza na kuyatumia katika kazi zao za kila siku, ili kuleta *tija, ufanisi na mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma bora kwa wateja na wananchi kwa ujumla*.

Watumishi wa MWAUWASA kwa upande wao walieleza kuwa wamepokea mafunzo hayo kwa hamasa na kuahidi kuwa mabalozi wa mabadiliko ndani ya Mamlaka ili kuboresha utoaji huduma muhimu ya maji na usafi wa mazingira kwa wananchi.

Mafunzo hayo ni endelevu na yataendelea kutolewa kwa makundi tofauti ya watumishi kwa awamu.