News
BILIONI 22 KUBORESHA HUDUMA YA USAFI WA MAZINGIRA MWANZA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imesaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa kuboresha mfumo rahisi wa uondoshaji Majitaka katika maeneo ya milimani jijini Mwanza, kwa lengo la kuimarisha usafi wa mazingira na kulinda Ziwa Victoria.
Mkataba huo wa nyongeza wenye thamani ya Euro milioni 7.86 (Bilioni 22 TZS) umesainiwa baina ya MWAUWASA na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), ukishuhudiwa na viongozi wa Serikali walioongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Amir Mkalipa.
Mradi utawezesha upanuzi wa mtandao wa Majitaka katika maeneo ya Kiseke, Lumala na Ilemela kwa ulazaji wa kilomita 25 za mabomba, maunganisho mapya kwa takribani kaya 1,800 pamoja na Taasisi na majengo ya kibiashara, ujenzi wa kituo cha kusukuma Majitaka, ujenzi wa maabara maalum na ununuzi wa magari mawili ya kunyonya majitaka.
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Neli Msuya amewashukuru wadau wa maendeleo, Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na Umoja wa Ulaya (EU), akibainisha kuwa mradi huo ni matokeo ya sera na diplomasia njema ya Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema MWAUWASA itaendelea kusimamia mradi kwa umakini, kushirikisha jamii na kuhakikisha uendelevu wa uwekezaji huo, huku akitambua mchango wa Wizara ya Maji kupitia Mhe. Waziri Jumaa Aweso na Katibu Mkuu.
Katibu Mtendaji Jumuiya ya Afrika Mashariki - LVBC, Dkt. Masinde Bwire, amesema mradi huo unaotekelezwa kwa programu ya kikanda unalenga kudhibiti uchafuzi wa Ziwa Victoria ambalo ni rasilimali muhimu kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika maji, uvuvi, nishati na uchumi wa wananchi. Ameeleza pia imani yake kwa MWAUWASA katika kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa mafanikio.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Amir Mohamed Mkalipa, amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi na kuwataka wananchi kulinda miundombinu na kulipia bili za huduma kwa wakati ili huduma iwe endelevu.
Awali, mradi huo ulitekelezwa katika maeneo ya Kabuhoro, Pasiansi, Kilimahewa A & B, Mabatini, Igogo Sahara, Igogo Bugando, Kitangiri na Isamilo ya Nyakabungo.