News

Posted On: Oct, 24 2024

BODI YA WAKURUGENZI KUWASA YATEMBELEA MWAUWASA KUVUNA UZOEFU

News Images

Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama ( KUWASA ) imetembelea Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kwa lengo la kuvuna ujuzi na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali.

Katika ziara hiyo, KUWASA imetembelea vyanzo viwili vikuu vya uzalishaji maji Jijini Mwanza vya Capripoint na Butimba na kujionea namna shughuli za uzalishaji maji zinavyofanyika kuanzia Mwanzo hadi hatua ya mwisho ya kusambaza maji yaliyokwisha tibiwa kwenda kwa Wateja ( Wananchi).

Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya KUWASA, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Stewart Mathias Bulaya amepongeza uwekezaji uliofanywa na Serikali hasa katika matumizi ya Teknolojia inayoendesha mitambo ya chanzo cha maji Butimba.

Ugeni huo umepokelewa na Bodi pamoja na Menejimenti ya MWAUWASA ambapo akizungumza kwa niaba ya Bodi ya MWAUWASA Mjumbe wa Bodi Ellen Bogohe amesema ushirikiano huo ni muhimu na kwamba MWAUWASA ipo tayari kuendelea kubadilishana uzoefu na Mamlaka zingine ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kama ilivyo Nia ya Serikali na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Baada ya kutembelea Miradi ya Majisafi, hapo kesho KUWASA itapata nafasi ya kutembelea Miradi ya Usafi wa Mazingira inayosimamiwa na MWAUWASA.