News
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YARIDHISHWA NA MRADI WA BUTIMBA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi wa Maji utakaozalisha lita milioni 48 za maji kwa siku unaojengwa eneo la Butimba Jijini Mwanza wenye thamani ya shilingi bilioni 69.
Hayo yamedhihirishwa Januari 13, 2023 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Athuman Maige (Mb) wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo wa Butimba.
"Kwa niaba ya Kamati tumeridhishwa na hali tuliyoishuhudia, tumeona kazi inafanyika, mradi unakwenda vizuri na ni matumaini yetu kero ya maji kwa wakazi wa Mwanza inakwenda kutatuliwa," amesema Mhe. Maige.
Hata hivyo, Kamati imeielekeza Wizara kuongeza usimamizi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) alipokea maelekezo ya Kamati na ameihakikishia kuwa Wizara itaongeza usimamizi ili mradi ukamilke inavyopasa.
"Sisi kama Wizara tumepokea maelekezo ya Kamati na tunaahidi kutekeleza yote yaliyoagizwa ili azma ya Rais wetu mpendwa Mhe. Dokta Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama wa Mwanza ndoo kichwani inatimia," amesema Mhandisi Mahundi.
Amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza na kwamba Wizara itahakikisha nia hiyo inafikiwa bila kuwepo kwa vikwazo.