News
KUWASA YAFURAHISHWA NA MIRADI YA USAFI WA MAZINGIRA MWAUWASA

Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama ( KUWASA ) imekamilisha ziara ya siku mbili kwa kutembelea Miradi ya Usafi wa Mazingira inayosimamiwa na MWAUWASA.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Mradi wa Mfumo rahisi wa uondoshaji Majitaka maeneo ya milimani (Simplified Sewerage System - SSS) eneo la Kilimahewa pamoja na Mabwaya ya kuchakata na kutibu Majitaka yaliyopo eneo la Butuja ( Sabasaba ) Jijini Mwanza.
"Tumejifunza mambo mengi kupitia ziara hii na tunaendelea kupongeza jitihada hizi za Serikali kwa uwekezaji huu, mradi huu wa uondoshaji Majitaka maeneo haya ya milimani ni wa mfano wa kuigwa" amebainisha Mwenyekiti wa Kamati hiyo Stewart Mathias Bulaya.
"Tunaamini mradi huu umepunguza uwezekano wa kutokea kwa Magonjwa ya mlipuko kwa Wananchi kwa asilimia kubwa, tunawapongeza MWAUWASA na uzoefu huu tutaenda kuutumia ili kuendelea kuboresha huduma katika sekta hii" amesema Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Simon Peter Cheyo.
Naye Mjumbe wa Bodi ya MWAUWASA Ellen Bogohe ameipongeza Bodi hiyo kwa ziara ya mafunzo na kusisitiza kuendeleza ushirikiano na kutumia ujuzi walioupata kwenda kuboresha zaidi huduma kwa Wakazi wa Kahama.
"Hongereni sana kwa ziara hii, kwa 'commitment' mliyoionesha kwenye ziara hii ninaamini Wana Kahama wataenda kunufaika zaidi na uzoefu mlioupata hapa MWAUWASA na kwa pamoja tutafanikisha azma ya Serikali na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani " amesisitiza.