News
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) inaendelea na uboreshaji wa huduma ya maji kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa kuleta matokeo ya haraka (Qui

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) inaendelea na uboreshaji wa huduma ya maji kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa kuleta matokeo ya haraka (Quick wins).
Moja ya eneo linalonufaika na mradi ni Kata ya Luchelele ambako shughuli za uchimbaji na ulazaji wa mabomba zinaendelea.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi wa Usambazaji maji na Usafi wa Mazingira wa MWAUWASA, Mhandisi Robert Lupoja ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa milioni 855 ambazo zitatumika kuongeza ukubwa wa bomba na kuongeza wingi wa maji kwa ajili ya kuboresha huduma ya majisafi katika Kata ya Luchelele.
"Mradi unahusisha kuongeza ukubwa wa bomba kutoka inchi 4 hadi inchi 10 kwa umbali wa kilomita 2, ulazaji wa bomba la inchi 8 kwa umbali wa kilomita 3, ulazaji wa bomba la inchi 6 kwa umbali wa kilomita 5 pamoja na ulazaji wa bomba kwa kilomita 1 kwa ajili ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi," amesema
Mhandisi Lupoja ametoa rai kwa wananchi wa Luchelele kuwa walinzi wa miundombinu ya maji ili mradi unufaishe wananchi kama ilivyopangwa.
"Kila mwananchi ni vyema akalinda miundombinu hii ili itupe matokeo chanya kama ilivyo sanifiwa," ameeleza
Diwani wa Kata ya Luchelele, Mhe. Vincent Lusana ameishukuru MWAUWASA kwa kuanza utekelezaji wa mradi katika kata hiyo na kusema wananchi wana matumaini makubwa na utekelezaji wa mradi huo wa uboreshaji.
"Tunaamini mradi huu utakapokamilika, changamoto ya upatikanaji wa maji zitapungua na tutaneemeka na utekelezaji wa mradi huu, tunaipongeza MWAUWASA na tuko tayari kutoa ushirikiano tutakapohitajika," amesema