News
MHA. KUNDO AENDESHA KIKAO NA VIONGOZI SEKTA YA MAJI MWANZA
MHA. KUNDO AENDESHA KIKAO NA VIONGOZI SEKTA YA MAJI MWANZA.
- Asisitiza Matumizi ya Mita za _Prepaid_
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ameanza rasmi ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Mwanza ambapo amekutana na viongozi wa Sekta ya Maji kujadili masuala mbalimbali kuhusu huduma ya maji.
Katika kikao hicho, Mhandisi Kundo amesisitiza msimamo wa Serikali unaotokana na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya mita za malipo kabla (prepaid meters) ili kuongeza uwazi na kuondoa malalamiko ya Wateja kuhusu bili za maji.
Ameagiza Viongozi hao kusimamia kikamilifu mchakato wa upatikanaji na ufungaji wa mita hizo na kuongeza kuwa Serikali inaunga mkono mifumo ya ubia ili kurahisisha upatikanaji wa mita na kuongeza ufanisi katika huduma ya maji.
Aidha, amekumbusha kuwa miradi yote ya maji iliyoanzishwa inapaswa kupewa kipaumbele cha kukamilishwa.
Amegusia pia suala la upotevu wa maji unaosababishwa na wizi, uvujaji wa miundombinu, matumizi yasiyo sahihi pamoja na ubovu wa mita, akisisitiza hatua ziendelee kuchukuliwa kudhibiti hali hiyo akieleza matumizi ya mita za Malipo kabla (prepaid meters) kuwa miongoni mwa suluhu za changamoto hiyo.
Akisoma taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mkurugenzi wa huduma kwa Wateja Salustia Kusekwa amesema Mamlaka tayari ilianza mchakato wa ufungaji wa mita hizo kwa baadhi ya Wateja kwa majaribio na kwamba ipo katika hatua za makubaliano na Wazabuni kwaajili ya kupata mita na kuwafungia Wateja wengi zaidi.
Awali, akizungumza katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Naibu Waziri amesema Sekta ya Maji itaendelea kushirikiana na mkoa kutatua changamoto za maji, akibainisha kuwa licha ya Mwanza kuwa na chanzo cha uhakika cha maji cha Ziwa Victoria, ongezeko la kasi la watu linaongeza mahitaji ya maji.