News

Posted On: Sep, 17 2025

MHANDISI MWAUWASA AGUNDUA NJIA MBADALA WA KUTIBU MAJI KWA KUTUMIA MIMEA YA ASILI

News Images

Mhandisi *Josephat Ilunde* wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) ameandika historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza duniani kufanya utafiti na kugundua teknolojia mpya ya kusafisha na kutibu maji kwa kutumia mimea ya asili *(Water Purification and Disinfection Using Locally Plant Materials).*

Tafiti hizo zimehakikiwa na kuthibitishwa kitaalamu na hatimaye kupata *hati miliki (Patent)*, sambamba na kukubaliwa na kusubiri kuchapishwa katika *jarida la kimataifa la kisayansi (Journal of Web Science - PLOS ONE)* nchini Marekani.

Teknolojia hiyo mpya imetambuliwa kama mbadala salama wa matumizi ya kemikali ya chlorine katika hatua za uchujaji na usafishaji wa maji, kwa kuwa ni *rafiki wa mazingira* na inalingana na mwelekeo wa dunia kuhusu matumizi endelevu ya rasilimali za asili.

Kupitia mafanikio hayo, Eng. Ilunde ambaye amehitimu Shahada ya Umahiri katika fani ya *Hydrolojia na Uhandisi wa Rasilimali za Maji (Master’s Degree in Hydrology and Water Resources Engineering)*, ametunukiwa *cheti cha heshima* pamoja na zawadi kama *Mwanafunzi bora katika ufaulu wa masomo na uvumbuzi (Best Student in Academic Performance & Top Student in Research and Innovation)*, katika *Shule Kuu ya Sayansi ya Rasilimali Vitu, Nishati, Maji na Mazingira* ya Chuo Kikuu cha Nelson Mandela African Institution of Science and Technology - (NM-AIST).

Bodi ya Wakurugenzi ikiongozwa na Mhe. Christopher Gachuma , Menejimenti na Wagumishi wa MWAUWASA wamempongeza Eng. Ilunde kwa bidii na ubunifu wake wenye tija. Ugunduzi huu utachangia katika kuboresha huduma ya maji safi kwa wananchi na kuchochea maendeleo endelevu katika sekta ya maji hasa kwa kupunguza matumizi ya kemikali.