News

Posted On: May, 29 2024

MKURUGENZI MWAUWASA AONGOZA WATUMISHI OPARESHENI MAALUM YA MTAA KWA MTAA

News Images

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Ndg. Neli Msuya ameongoza watumishi wa MWAUWASA katika zoezi maalum la ufuatiliaji wa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji mitaani.

Zoezi hilo lilianza rasmi hapo jana Mei 28, 2024 katika maeneo yanayohudumiwa na Kanda ya Nyakato na linaendelea katika kanda hiyo hadi Mei 30, 2024 na kisha litahamia katika kanda nyingine.

"Tupo mitaani na watumishi wenzangu kufuatilia hali ya upatikanaji wa huduma ya maji, kukagua ufanisi wa mfumo wa usambazaji maji kwa maana ya bomba na dira za maji, kuzungumza na wateja na kusikiliza maoni yao, kufanya maboresho madogo madogo ya kimfumo sambamba na kufuatilia madeni ya muda mrefu," amesema Ndg. Neli.

Ndg. Neli amesema MWAUWASA inaendelea na jitihada za kuhakikisha huduma ya maji katila maeneo yote inayohudumia inaimarika kama ilivyo azma ya Serikali kupitia Wizara ya Maji.

Mkurugenzi Neli amewakumbusha wateja kuhakikisha wanalipa ankara zao kwa wakati ili kuiwezesha MWAUWASA kuendelea kuboresha huduma.

"Lengo na dhamira yetu ni kuona huduma inaimarika na tunawaohudumia wanafikiwa kikamilifu lakini pia tupo mtaani kuwakumbusha wateja wetu wajibu wao wa kulipa ankara na pia tunafuatilia wadaiwa sugu kuhakikisha nao wanalipa malimbikizo ya madeni yao," amesema.

Zoezi hilo linakwenda sambamba na utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya maji, usomaji shirikishi wa dira, namna ya kutoa taarifa kwa MWAUWASA.