News

Posted On: Feb, 23 2021

MWAROBAINI KERO YA MAJI ILEMELA WAPATIKANA

News Images

MWAROBAINI KERO YA MAJI ILEMELA WAPATIKANA

Kwa kutambua kero ya upatikanaji wa majisafi na salama inayowakabili wananchi wa Ilemela hususan Kata ya Buswelu, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza inatekeleza mradi wa shilingi bilioni 5.1 ili kuondokana na adha hiyo.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoani Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele iliyolenga kukagua ujenzi wa tenki la maji la lita milioni 3 linalojengwa kwenye kata hiyo.

Dkt. Lalika alisema mradi huo wa tenki ni miongoni mwa miradi ambayo ilitengewa fedha Mwaka wa fedha 2019/2020 ikiwa ni utekelezaji wa sera ya Serikali ya kuhakikisha wananchi hawatembei umbali mrefu kufuata huduma ya maji.

“Serikali ya Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli ilijipambanua vyema kutetea wananchi wake na kwamba mwananchi hapaswi kutembea zaidi ya mita 400 kufuatilia huduma ya maji,” alisema Dkt. Lalika.

Alifafanua kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mwananchi anapata muda mwingi wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo ili kujiongezea kipato na hivyo kukuza uchumi wake binafsi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Alisema anatambua miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na MWAUWASA kwenye wilaya hiyo na aliipongeza kwa jitihada zake katika kusimamia ujenzi wa miradi ya maji kwa niaba ya Serikali ambapo alisema kupitia miradi hiyo kero ya maji inakwenda kuwa historia.

“Natambua MWAUWASA inatekeleza miradi mingine ya maji Wilayani Ilemela mbali na huu tuliotembelea leo ambayo ni pamoja na Mjimwema, Nyasaka, Nyamhongolo, Kabusungu, Kabangaja, Igalagala na Kayenze, ninaamini kero ya maji itabaki historia,” alisema Dkt. Lalika.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi, Mhandisi Msenyele alisema unagharamiwa na Serikali kwa asilimia Miamoja kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa wahisani ambao ni Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa.

Alisema ujenzi wa tenki hilo ulianza rasmi Septemba, 2020 na kwamba unatarajiwa kukamilika ifikapo Mwezi Julai 2021. Alifafanua kuwa mradi unahusisha ujenzi wa tenki la lita milioni tatu, ulazaji wa bomba urefu wa kilomita 14 na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji kufika kwenye tenki ambacho kinajengwa kwenye eneo la Kiseke Jeshini.

Alibainisha kwamba kukamilika kwa mradi huo wa tenki kutanufaisha wananchi wa maeneo ya Buswelu, Lukobe, Kigala, Nsumba, Kahama, Bujigwa, Nyamadoke na Ilalila.

Mhandisi Msenyele alisema mradi huo ni sehemu ya Programu ya Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Jiji la Mwanza (LV WATSAN).

CAPTIONS

  1. Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele wakikagua ujenzi wa mradi wa maji unaojengwa kwenye Kata ya Buswelu.
  2. Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele (wa pili kushoto) akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika (kushoto) ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji unaojengwa kwenye Kata ya Buswelu.
  3. Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika akipata maelezo ya ujenzi wa tenki la lita milioni tatu linalojengwa wilayani humo kutoka kwa Mtaalam Mshauri, Mhandisi Andrew Seleli