News
MWAUWASA NA VEI KUSHIRIKIANA, MAPAMBANO DHIDI YA UPOTEVU WA MAJI
Katika kuendelea kuhakikisha huduma ya maji Jijini Mwanza inazidi kuimarika Shirika la Maji la Uholanzi (Vitens Evides International - VEI) imekabidhi vyombo vya usafiri aina ya pikipiki kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA kwa lengo la kuunga mkono jitihada za udhibiti wa upotevu wa Maji.
Zoezi hilo limefuatia baada ya VEI na MWAUWASA kusaini hati ya makubaliano (Memorandum of Understanding - MOU) hii leo Septemba 25, 2024 kuhusu ushirikiano wa pamoja katika suala la udhibiti wa upotevu wa Maji chini ya Mradi wa "Usalama wa Maji na uimara wa hali ya hewa kwa Maendeleo ya Mijini" (Green and Smart Cities - 'SASA').
Akizungumza wakati wa zoezi la makabidhiano hayo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Neli Msuya amesema ushirikiano huo utasaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi kwa kupunguza upotevu wa maji na hivyo maji yanayozalishwa yataweza kuwafikia wananchi kwa wingi.
"Vyombo hivi vya usafiri vitaenda kuwawezesha Mafundi wetu kuzunguka maeneo mbalimbali na kukagua miundombinu yetu kwa urahisi na haraka hivyo watakapobaini mivujo ama changamoto yoyote itakua rahisi kuifikia na kudhibiti kwa haraka" Ameeleza Mkurugenzi Neli.
Kwa upande wake Meneja Miradi wa VEI, Andries Van Eckeveld amesema VEI itaendelea kushirikiana na MWAUWASA kuunga mkono jitihada za udhibiti wa upotevu wa Maji kwa njia mbalimbali ikiwemo kujengeana na kubadilisha uwezo na uzoefu kwa Watumishi, usimamizi wa mita za maji pamoja na mambo mengine yanayosaidia kudhibiti upotevu wa Maji yanayozalishwa.
Mradi wa Green and Smart Cities 'SASA' umeanza kutekelezwa mwezi Juni 2024 na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2026 ukihusisha masuala mbalimbali ikiwemo Usafi wa Mazingira na Maboresho ya huduma ya Maji kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) ukitekelezwa katika mikoa ya Mwanza, Tanga na Pemba.