News
MWAUWASA YAWATAMBUA WATEJA WAKE - KILELE CHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imeadhimisha kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa MajiHouse Oktoba 10 2025.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Neli Msuya amesema MWAUWASA itaendelea kuboresha huduma zake siku hadi siku kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan wa maeneo ya pembezoni. Amesema MWAUWASA imefanikiwa kuongeza wateja wapya wapatao 13,000 baada ya Chanzo cha maji Butimba kuanza kufanya kazi.
Aidha, amesisitiza kuwa Wateja ni kiungo muhimu kwa uhai na mafanikio ya Mamlaka, hivyo MWAUWASA itaendelea kuwashirikisha katika kila hatua ya kuboresha huduma. Amewaomba kuendelea kutoa ushirikiano kwa kulipa bili kwa wakati, kutoa taarifa za upotevu wa maji pamoja na maoni ya kuboresha huduma. Pia amewakumbusha kuchangamkia Ofa ya kurejeshewa huduma kwa wateja waliositishiwa huduma kwa kushindwa kulipa Ankara ambapo Ofa hiyo itafika ukomo tarehe 31 Oktoba 2025.
Katika hafla hiyo, MWAUWASA pia imewatambua wateja waliotoa ushirikiano kwa mambo mbalimbali ikiwemo utoaji wa taarifa muhimu kuhusu huduma, kama vile upotevu wa maji. Wateja wamekabidhiwa Tuzo na Mkurugenzi Mtendaji. Aidha, Meneja wa Huduma kwa Wateja, Sia Mrema amewashukuru Wateja kwa mchango wao na kuwaomba kuendelea kuwa mabalozi kwa wengine.
Mkurugenzi pia amewakumbusha wananchi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025 kwa ajili ya kuchagua viongozi bora kwa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wao, wateja waliopata fursa ya kuzungumza waliishukuru MWAUWASA kwa jitihada inazofanya na kuahidi kuendeleza ushirikiano na kuwa mabalozi wa huduma bora kwa wengine.