News
MWENGE WA UHURU WAKAGUA MRADI WA UJENZI WA MATENKI YA MAJI

Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso wamepongezwa kwa juhudi kubwa katika kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya maji nchini.*
Pongezi hizo zimetolewa leo, *tarehe 25 Agosti 2025*, na *Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Ismail Ali Ussi*, alipokagua *mradi mkubwa wa ujenzi wa matenki matano, ulazaji wa mabomba makuu na vituo viwili vya kusukuma maji* katika eneo la *Sahwa*, jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Ndugu Ismail aliipongeza *Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA)* kwa *uongozi bora, usimamizi madhubuti na uzalendo wa hali ya juu* katika utekelezaji wa mradi huo chini ya *mkandarasi Sinohydro Corporation Ltd JV M/s Highland Build Company Ltd.*
“Nizidi kumpongeza Mhe. Rais amewatendea haki Wanamwanza kwa mradi huu mkubwa. Kama mngeshindwa kutuleta hapa, msingetutendea haki kuona kazi hii adhimu ya sekta ya maji,” alisema.
Aliongeza: “Nimetembelea mamlaka nyingi zinazohusika na miundombinu ya maji nchini, lakini kwa kweli huu ni *baba lao*.”
Kwa upande wake, *Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA*, Bi. *Neli Msuya*, alisema kuwa *mradi huu ulianza Desemba 24, 2024 na unatarajiwa kukamilika Desemba 24, 2026*, ambapo utahudumia wakazi zaidi ya *450,000* katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza.