News

Posted On: Nov, 17 2025

NYAMHONGOLO WAKUMBUSHWA UMUHIMU WA KULINDA MIUNDOMBINU YA MAJI

News Images

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imeendelea na jitihada za kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza miundombinu ya maji, ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na endelevu.

Katika jitihada hizo, MWAUWASA kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Ilamba A, imeandaa kikao kifupi cha uelimishaji kwa wananchi tarehe 15 Oktoba 2025, kilichofanyika katika eneo la mlima lilipo tanki la maji la Nyamhongolo katika mtaa huo.

Kikao hicho kililenga kuonya na kuelimisha wakazi dhidi ya tabia ya kuchimba mawe karibu na tanki la maji, jambo linalotishia usalama wa miundombinu na uhakika wa huduma ya maji kwa wananchi.

Sambamba na wananchi kuelezwa kuwa uchimbaji wa mawe husababisha mitikisiko inayoweza kusababisha nyufa kwenye tanki, hatari kwa usalama wa watu na makazi, na kupunguza muda wa matumizi ya miundombinu hiyo, pia walikumbushwa kuwa ni kosa la jinai kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo uchimbaji kwenye maeneo ya miundombinu ya maji kwa mujibu wa Sheria ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya mwaka 2019.

MWAUWASA inaendelea kukumbusha Jamii kujiepusha kufanya shughuli za kibinadamu kama uchimbaji, kilimo na shughuli nyingine kama hizo maeneo ya vyanzo au miundombinu ya maji ili kulinda miundombinu hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.