News

Posted On: Feb, 13 2026

SERIKALI KUIMARISHA HUDUMA YA MAJI KUPITIA MIRADI YA KIMKAKATI

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Kundo Mathew, ameendelea na ziara yake MWAUWASA kwa siku ya pili kwa kutembelea mradi wa ujenzi wa matenki ya kuhifadhia maji Buhongwa, Fumagila na Nyamazobe pamoja na kituo vya kusukuma maji Sahwa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Kundo amesema Sekta ya Maji inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ili kufanikisha Gridi ya taifa ya maji akirejea hotuba ya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Bungeni, kwa kuzingatia utekelezaji wa sera ya maji kwa vitendo unaolenga upatikanaji wa maji kupitia vyanzo, uboreshaji wa miundombinu ya usambazaji pamoja na gharama nafuu ya maji kulingana na maisha ya wananchi.

Ameeleza kuwa awali maji yalikuwa yanazalishwa lakini hayakuwafikia wananchi kikamilifu, hali itakayobadilika kupitia ujenzi wa matenki hayo. Aidha, amesifu kasi ya mkandarasi pamoja na usimamizi madhubuti wa MWAUWASA huku akimwelekeza Mkandarasi kuhakikisha anazingatia Maslahi ya wafanyakazi kwa kuwapatia stahiki zao kadri taratibu zinavyoelekeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Neli Msuya, amesema miradi hiyo itatoa matokeo ya chanzo kipya cha Butimba kwa kupokea maji kutoka chanzo hicho, ambapo matenki yamejengwa maeneo ya juu na yaliyokuwa na changamoto ya maji, hivyo kunufaisha wananchi moja kwa moja.

Amesema MWAUWASA itaendelea kusimamia mradi kikamilifu hadi ukamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya kazi kwa niaba ya mkandarasi, Mhandisi Mkazi Raphael Joseph amesema mradi umefikia asilimia 40, unahusisha ujenzi wa matenki matano (Buhongwa, Fumagila, Nyamazobe, Kisesa na Usagara), vituo viwili vya kusukuma maji vya Sahwa na Butimba pamoja na ulazaji wa mabomba makuu ya kusambaza maji kwa urefu wa kilomita 40.5.

Mradi unatarajiwa kukamilika Desemba 2026.