News

Posted On: May, 29 2024

WANANCHI WAPONGEZA JITIHADA ZA MWAUWASA

News Images

Wananchi wa Mtaa wa Stone Town Kata ya Kahama Wilayani Ilemela wameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kwa jitihada zake za kuimarisha huduma ya maji katika eneo hilo.

Wametoa pongezi hizo mbele ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Ndg. Neli Msuya Mei 28, 2024 wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezwaji wa mradi wa matokeo ya haraka (quick win) katika maeneo ya Kahama, Buswelu na Nyamadoke.

"Mkurugenzi unafanya kazi kubwa, unatekeleza dhamira ya Serikali kwa vitendo. Tunakupongeza kufanya ziara za kukagua maendeleo ya mradi huu na ulituahidi na kweli tunashuhudia," amesema Ramadhan Matoke, Mwenyekiti wa Mtaa Stone Town

Aidha, wananchi hao walipongeza jitihada za Mbunge wa Ilemela Mhe. Dkt. Angelina Mabula za kuwaletea maendeleo kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ambayo ameendelea kuipambania ikiwemo mradi huo wa maji.

Katika ziara hiyo Ndg. Neli alipata fursa ya kuzungumza na wananchi ikiwa ni utaratibu aliyojiwekea wa kuzungumza na wanufaika wa mradi kila anapotembelea kukagua hatua za ujenzi wa mradi.

Mkurugenzi Neli aliwasisitiza mafundi wa MWAUWASA wanaosimamia mradi kuhakikisha mradi unakamilika kama alivyoelekeza hapo awali bila kuwa na kisingizio chochote.

"Meneja wa Kanda anza taratibu za kuwaunganisha wananchi wa Mtaa huu kwani hadi sasa mradi unakwenda kama tunavyotarajia. Nawasihi wananchi tushirikiane kulinda na kutunza miundombinu hii ili tuweze kunufaika na mradi," alisisitiza Mkurugenzi Neli.

Ndg. Neli aliwakumbusha wananchi kufanya malipo ya MWAUWASA kwa kutumia namba maalum ya malipo (control number) ili kuepuka kutapeliwa.

"Nitawaleta kwenu wataalam wa masuala ya Jamii wa MWAUWASA ili kuendelea kuwapatia elimu ya masuala mbalimbali ya huduma za Mamlaka," alisema Ndg. Neli.

Ziara hiyo ya Mkurugenzi ya ukaguzi wa mradi ni ya pili katika eneo hilo ndani ya mwezi huu ambapo hapo awali Mei 21.2024, alitembelea mradi na kuelekeza ifikapo tarehe 30 Mei, 2024 uwe umekamilika na wananchi waunganishwe na huduma.