News
WARSHA YA KUJADILI MABORESHO MPANGO WA USALAMA WA MAJI UNAOZINGATIA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Neli Msuya amefungua rasmi warsha maalum ya kupitia na kuboresha Mpango wa Usalama wa Maji unaozingatia Uhimilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi*, katika ukumbi wa Vigmark Hotel, Shinyanga.
Warsha hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa MWAUWASA kutoka kada mbalimbali, pamoja na wataalam kutoka Taasisi mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bodi ya bonde la maji ziwa Victoria, TARURA, TANESCO, RUWASA, Mamlaka ya hali ya hewa, Ofisi ya mkemia Mkuu wa Serikali, NEMC, na Maabara ya ubora wa maji. Vilevile, warsha hiyo inahusisha wadau wa maendeleo kutoka Shirika la ushirikiano wa kimataifa la Ujerumani (GIZ).
Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo, Bi. Neli amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wadau wote waliopo kwa kutoa maoni, ujuzi na uzoefu wao ili kuhakikisha mpango huo unakuwa wa kisasa, unaotekelezeka na unaojibu changamoto za sasa na za baadae.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huu ni muhimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho*, hivyo unatakiwa kutekelezwa kikamilifu Kwa ushirikiano wa sekta zote kwa dhamira ya kweli ya kulinda rasilimali za maji dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Warsha hiyo inafanyika kwa siku nne na imeandaliwa kwa ushirikiano baina ya MWAUWASA na Shirika la maji la Uholanzi - VEI chini ya Wizara ya Maji.