News

Posted On: Jul, 25 2022

WAZIRI AWESO AZUNGUMZIA CHANGAMOTO YA MAJI MWANZA

News Images

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewasihi wakazi wa Mwanza hususan wa maeneo ya miinuko kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji.

Waziri Aweso amesema hayo hivi leo alipotembelea Kituo cha Kusukuma Maji Mabatini (Mabatini Booster Station) Jijini Mwanza ili kujionea hitilafu ya mitambo iiyosababisha upungufu wa maji.

"Nimekuja kuona hali ya upatikanaji wa maji Jijini Mwanza kufuatia malalamiko ya wananchi kupitia wawakilishi wao," amesema Waziri Aweso.

Amesema Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemuelekeza kuwa hataki kuona wala kusikia eneo lolote linataharuki ya kukosekana kwa huduma ya maji.

"Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametuelekeza hataki kusikia wala kuona wananchi wake wanataabika kwa kukosa huduma ya maji, nipo hapa kufuatilia maelekezo haya," amesema Waziri Aweso.

Waziri Aweso amekutana na Bodi na Watendaji wa Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA) na ameelekeza masuala muhimu ya kuzingatia ili wananchi wapate huduma ikiwa ni pamoja na kukiagiza Kitengo cha usambazaji maji kuhakikisha kinaandaa utaratibu mzuri wa migao ya maji katika kipindi hiki cha mpito.

Amesema hitilafu hiyo iliyojitokeza Jijini Mwanza imepelekea kuwa na upungufu wa takriban lita milioni 10 za maji ambayo kwa kiasi kikubwa imeathiri upatikanaji wa huduma ya maji hususan kwenye maeneo ya miinuko.