News

Posted On: Feb, 13 2026

WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA UBORESHAJI WA MFUMO WA USAMBAZAJI MAJI - MWANZA

News Images

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameweka jiwe la msingi la Mradi wa Uboreshaji wa Mfumo wa Usambazaji wa Maji unaolenga kuboresha upatikanaji wa Majisafi kwa wakazi wa Jiji la Mwanza. Mradi huo unahusisha ujenzi wa matenki matano ya maji yenye jumla ya ujazo wa lita Milioni 31 yatakayojengwa katika maeneo ya Buhongwa, Fumagila, Nyamazobe, Kisesa na Usagara.

Aidha, mradi unajumuisha ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji katika maeneo ya Sahwa na Butimba pamoja na ulazaji wa mabomba makuu ya kusafirisha maji yenye urefu wa kilomita 40.5.Ukigharimu TZS Bilioni 46.2

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili ihakikishe inatekelezwa kwa ufanisi, kwa viwango vinavyotakiwa na kukamilika ndani ya muda uliopangwa, kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma bora kwa wakati.

Ameeleza kuwa makubaliano ya Serikali ni kuhakikisha fedha za miradi ya maji zinatolewa kwa wakati ili miradi ite­kelezwe bila kuchelewa, akisisitiza kuwa maji hayana mbadala. Aidha, amemuelekeza mkandarasi kufanya kazi kwa kasi, ikiwezekana usiku na mchana, kwa kuwa fedha za ujenzi wa mradi huo tayari zipo.

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amesema Wizara ya Maji haitakuwa kikwazo cha utekelezaji wa miradi ya maji, akisisitiza kuwa mkandarasi hana kisingizio kwani fedha zote za mradi zipo, na kuahidi kuwa miradi itakamilika kwa muda uliopangwa.

Aidha, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Neli Msuya, akieleza kuwa licha ya yeye kuwa mwanahabari tofauti na ilivyozoeleka, amethibitisha uwezo mkubwa wa kiuongozi na kwamba kama Waziri wake, anaridhishwa kikamilifu na utendaji wake.

Awali, akisoma taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Neli Msuya, amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu ni sehemu ya mkakati wa kuongeza tija ya Mtambo wa Maji wa Butimba ambao baada ya kukamilika ulikuwa ukitoa huduma kupitia mfumo wa zamani usiotosheleza mahitaji ya sasa.

Ameeleza kuwa ujenzi wa matenki katika vilele vya milima inayoizunguka Mwanza utaimarisha uwiano wa usambazaji wa maji.